Kutokana na taarifa zilizotolewa na gazeti la HabariLeo la tarehe 19 Juni ukurasa wa 4, na kurudiwa kwenye tahariri ya gazeti hilo la tarehe 20 Juni ukurasa wa 6, HakiElimu inapenda kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusu maana, malengo na ukweli wa takwimu za ujenzi wa nyumba za walimu zilizotumika kwenye tangazo letu kwa wananchi.
Tangazo ujumbe wa maneno yafuatayo:-
..“.Mwaka 2008, Serikali ilipanga kujenga takriban nyumba za walimu 22,000, lakini zilizojengwa ni kama nyumba 300; yaani asilimia moja tu. Kutokana na upungufu wa nyumba za walimu, walimu wachache waliopo shuleni wanalazimika kufundisha kwa muda mrefu na hata kufundisha masomo wasiyoyasomea. Hali hii inadumaza elimu. Kuna upungufu mkubwa wa nyumba za walimu. Japo hazitoshi, ni muhimu sasa Serikali itekeleze ahadi ya kujenga nyumba 22,000 za walimu, kama mpango wa MMEM unavyosema, kwa mwaka 2010/ 2011”.
Tunapenda wananchi wafahamu ukweli ufuatao:-
1. Chanzo cha takwimu zilizotumiwa kwenye tangazo hilo ni Ripoti ya Serikali ya Utekelezaji wa MMEM II kwa mwaka 2007/2008 yenye jina la “Primary Education Development Programme II (2007-2011): Annual Performance Report FY- 2007/2008) iliyotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na TAMISEMI mwezi Agosti, 2008. Katika ukurasa wa 11, kipengele 2.1.2 kinachohusu “Miundombinu ya shule” (School infrastructure), aya ya kwanza. Serikali inatamka wazi kuhusu idadi ya nyumba ilizojenga kulinganisha na malengo yake. Tunanukuu:
“…The target for 2007/8 under this component was to construct 5, 732 pre-primary classrooms, 10,753 primary classrooms and 21,936 teachers’ houses in rural and remote areas. Providing teachers with houses is a positive incentive and motivation for retaining them in their working areas. In the year under review a total of 1, 263 classrooms, 277 teachers’ houses...were constructed..”
Ikimaanisha kwamba (kwa tafsiri yetu):
“…shabaha ya serikali kwa mwaka 2007/2008 ilikuwa ni kujenga madarasa 5,732 ya elimu ya awali. Madarasa 10,753 kwa shule za msingi na nyumba za walimu 21,936 katika maeneo ya vijijini na yaliyo pembezoni zaidi. Kuwapatia nyumba za walimu ni kichocheo chanya na motisha muhimu ya kuwabakiza walimu katika maeneo yao. Kwa mwaka wa mapitio (2007/8), jumla ya madarasa 1, 263 na nyumba za walimu 277 zilijengwa….”
2. HakiElimu katika tangazo lake haikuongelea ujenzi wa nyumba za walimu kwa kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya nne, isipokuwa imezungumzia utekelezaji wa MEMM II (2007-2011), tena kwa kipindi cha mwaka 2008 tu.
3. Katika tangazo hilo, HakiElimu haijasema kwamba kuna uhaba wa nyumba 22,000 kama mwandishi wa gazeti hilo alivyobainisha. Bali imesema, Serikali ilipanga kujenga idadi ya nyumba hizo, kama nyaraka zake, MMEM II na ripoti ya Serikali ya utekelezaji wake kwa mwaka 2007/2008 (Primary Education Development Programme II (2007-2011): Annual Performance Report FY- 2007/2008) zinavyobainisha.
4. Vilevile, tangazo la HakiElimu halijasema Serikali ya awamu ya nne kwa kipindi chote cha utawala wake imemudu kujenga idadi ya nyumba za walimu zipatazo 300 tu, bali imesema serikali imejenga kiasi hiki cha nyumba za walimu kwa kipindi cha mwaka 2008 tu. Ripoti tajwa inathibitisha hilo.
5. HakiElimu siku zote inazingatia ukweli na ushahidi wa kitakwimu kutoka kwenye nyaraka za Serikali yenyewe, tafiti zake na za wadau mbalimbali. Pia kwa kutembelea na kuona hali halisi kabla ya kutoa ujumbe wowote.
6. Lengo la tangazo la HakiElimu ni kuonesha madhara yanayotokana na upungufu wa nyumba za walimu; ambayo ni pamoja na kuchangia walimu kadhaa kuacha kazi na kusita kwenda kufundisha hasa maeneo ya vijijini na yale ya pembezoni. Hii ni kutokana na kutokuwa na uhakika wa mahali pa kuishi. Ripoti ya serikali pia imebainisha hili. Katika tangazo hili, HakiElimu inaiomba Serikali kutenga pesa kwenye bajeti ya 2010/11 kwa ajili ya kujenga nyumba nyingine 22,000 za walimu kama ilivyopangwa kwenye MMEM II (kwa mwaka wa fedha 2010/11).
7. HakiElimu inatambua mchango wa mashirika mbalimbali katika ujenzi wa nyumba za walimu nchini na elimu kwa ujumla, lakini inaamini kuwa mchango huo hauzuii mipango na bajeti iliyotengwa na serikali kutekelezwa.
8. Dhima ya asasi za kiraia kamwe sio kupongeza serikali wala kulumbana nayo; na wala sio kupotosha umma. Ni kukuza na kupanua wigo wa demokrasia na ushiriki wa wananchi katika kuleta maendeleo. Wananchi siku zote wanafahamu na wanapaswa kuendelea kufahamu kwamba; moja ya kazi muhimu za asasi za kiraia ni kufuatilia utendaji wa serikali katika masuala yote yanayohusu maendeleo na ustawi wa wananchi.
No comments:
Post a Comment