Thursday, June 17, 2010

Harambee ya Mamlaka ya Elimu Kusaidia Wasiojiweza Kupitia M-Pesa


KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imeingia makubaliano na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambapo wananchi sasa wataweza kuchangia maendeleo ya elimu nchini kupitia huduma ya Vodafone M-Pesa.
Mkurugenzi wa Mauzo, Huduma za Kabla na Usambazaji wa Vodacom, Exaud Kiwali alisema jana kuwa mpango huo umefikiwa baada ya Vodacom Tanzania kuingia mkataba wa ushirikiano kati yake na TEA.
Vodafone M-Pesa ni huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa kutumia simu za mkononi ambayo hutolewa na Vodacom Tanzania kwa wateja wake kwenda mtandao mwengine wowote Tanzania.
Kiwali alisema kwamba mteja wa Vodacom aliyejisajili na huduma ya Vodafone M-Pesa sasa anaweza kuchangia fedha kwa kutuma mchango wake kwenda namba 300100.Alisema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Vodacom Tanzania wa kusaidia jamii katika sekta ya maendeleo ya elimu.
“Ikumbukwe kwamba hivi sasa Vodacom Tanzania kupitia Mfuko wake wa kusaidia jamii (Vodacom Foundation) ina programu maalum ya kukuza elimu na kupitia mfuko huo inatoa kompyuta na madawati pamoja na kujenga madarasa ya shule mbalimbali za sekondari hapa nchini”, alisema.
Vodacom Tanzania ina mkakati wa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu hapa nchini ili kukuza na kuboresha kiwango cha elimu.
Kwa kutumia huduma ya Vodafone M-Pesa, uchangiaji wa maendeleo ya elimu hivi sasa utakua umefanywa rahisi na Kiwali alitoa wito kwa Watanzania kutumia ipasavyo mpango huu.
Naye Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Ukuzaji Rasilimali wa Mamlaka ya elimu Tanzania Seif Mohamed aliishukuru Vodacom Tanzania kwa ushirikiano huo ambao alisema una lenga kukuza kiwango cha elimu hapa Tanzania.
“Kupitia huduma ya M- PESA, wachangiaji wa maendeleo ya elimu wataweza kuchangia moja kwa moja bila makato yeyote kwa mchangiaji au mpokeaji”, alisema.
Alisema kwa kuanzia michango yote itakwenda katika kampeni maalum ya kuchangia wanafunzi wenye ulemavu inayoendeshwa na mamlaka hiyo.
Mpango huu utawezesha watanzania wengi kushiriki kuchangia maendeleo ya elimu nchini popote walipo kupitia M-PESA.
‘Vodacom na Mamlaka ya Elimu Tanzania inawaomba watumiaji wa mtandao huo, kushiriki katika kampeni hii kwa kuchangia kupitia M-PESA”, alisistiza

No comments:

Post a Comment