Thursday, June 24, 2010

Idadi ya Watoto Wanaofanya Kazi za Kuajiriwa Imeongezeka Katika Nchi Za Kusini Mwa Jangwa la Sahara



Na Anna Nkinda - Nairobi

Idadi ya watoto wanaofanya kazi za kuajiriwa imeongezeka katika nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara kutoka milioni 49 kwa mwaka 2004 hadi kufikia milioni 58 kwa mwaka 2008.

Aidha ajira za watoto wenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 14 imeongezeka kwani mwaka 2000 ilikuwa milioni 48 sawa na asilimia 28.8, mwaka 2004 milioni 49 sawa na asilimia 26.4 na mwaka 2008 milioni 58 sawa na asilimia 28.4.

Hayo yamesemwa jana na Wangui Inimu ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taifa kutoka Shirika la kazi Duniani (ILO) nchini Kenya wakati akitoa ripoti ya kimataifa kuhusu hali ya ajira za watoto ilivyo kwa sasa kwa wadau mbalimbali wanaofanya kazi na watoto katika hoteli ya Pan Africa jijini Nairobi.

Akifafanua takwimu za watoto wote wanaofanya kazi hapa Dunia alisema kuwa hivi sasa wako milioni 215 na kati ya hao watoto milioni 115 wanafanya kazi ambazi siyo salama kwa maisha yao .

Watoto wenye umri wa kati ya miaka mitano hadi 14 katika nchi za Asia na Pacific kwa mwaka 2000 waliokuwa wameajiriwa ni milioni 127 sawa na asilimia 19.1, mwaka 2004 ni milioni 122 sawa na asilimia 18.8 na mwaka 2008 ni milioni 96 sawa na asilimia 14.8. Nchi za Latini Amerika na Visiwa vya Caribbean mwaka 2000 walikuwa watoto milioni 17 sawa na asilimia 16.1, mwaka 2004 milioni 11 sawa na asilimia 10 na mwaka 2008 milioni 10 sawa na asilimia 9.

Inimu alisema, “Katika takwimu za kimataifa watoto kati ya umri wa miaka mitano hadi 17 kwa mwaka 2000 waliokuwa wanafanya kazi za kuajiriwa ni 245,500,000 sawa na asilimia 16, mwaka 2004 ni 222,290,000 sawa na asilimia 14.2 na mwaka 2008 ni milioni 215,270,000 sawa na asilimia 13.6”.

Aliongeza kuwa idadi ya watoto ambao walikuwa wanaofanya kazi ambazo si salama kwa maisha yao wenye umri wa kati ya miaka mitano hadi 17 kwa mwaka 2000 ni 170,500,000 sawa na asilimia 11.1, mwaka 2004 walikuwa 128,380,000 sawa na asilimia 8.2 na mwaka 2008 ni 115, 310,000 sawa na asilimia 7.3.
Aliendelea kusema kuwa watoto waliokuwa wameajiariwa kati ya umri wa miaka mitano hadi 14 kwa mwaka 2000 walikuwa 186,300,000, mwaka 2004 walikuwa 170,380,000 na mwaka 2008 walikuwa 152,850,000.

“Kwa mwaka 2000 watoto wa kike waliokuwa wanafanya kazi za kuajiriwa walikuwa asilimia 15.2 na wa kiume asilimia 16.8, mwaka 2004 watoto wa kike walikuwa asilimia 13.5 wa kiume 14.9 na mwaka 2008 watoto wa kike walikuwa asilimia 11.4 na wa kiume asilimia 15.6” .
“Hivi ajira kwa watoto wa kike imepungua kwa asilimia 15 hii ni kutokana na asasi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali kuwaangalia kwa ukaribu zaidi na kuwasahau watoto wa kiume”, alisema.

Inimu alisema kuwa tatizo kubwa lililopo hivi sasa ni kuongezeka kwa ajira za watoto wa kiume ambapo zimeongezeka kwa asilimia 20 kwa watoto wa kati ya umri wa miaka 15 na 17 ambao wanaajiriwa kwa wingi na wanafanya kazi ambazo ni hatari kwa maisha yao. Aliongeza kuwa ajira za watoto hao kwa mwaka 2000 zilikuwa asilimia 17.8, mwaka 2004 asilimia 14.4 na mwaka 2008 asilimia 16.9.

Asilimia 60 ya watoto walioajiriwa wanafanya kazi za mashambani, asilimia 25.6 kazi za kutoa huduma, asilimia 7 kazi za viwandani na 7.5 wanafanya kazi zisizoeleweka .
Afisa huyo alizitaja sababu za kuongezeka kwa ajira za watoto kuwa ni umaskini unaozikabili familia nyingi jambo ambalo linawafanya wazazi wengi kuwatumia watoto wao kama mtaji wa kujipatia fedha za kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

No comments:

Post a Comment