Tuesday, September 21, 2010

SERIKALI: HAKUTA KUWA NA MGAWO WA UMEME

Kampuni ya Borodino kutoka nchini Urusi ya uwekezaji wa umeme imetia saini na Serikali ya Tanzania mkataba wa mradi wa umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji wenye uwezo wa kuzalisha 222 MV wenye thamani ya dola za Marekani milioni 700.

Makubaliano ya mkataba huo, yalitiwa saini jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya hiyo Razmik Tarverdyan katika ukumbi wa mkukutano wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam.

Mradi huo unaojengwa katika eneo la Rumakali ,mkoani Iringa unatarajiwa kukamilika mwaka 2018.

Akizungumzia kuhusu jijitahada za Serikali katika masuala ya umeme, Katibu Mkuu huyo, Jairo alisema wizara yake itahakikisha kuwa Tanzania haitarudi nyuma katika masuala ya nishati hiyo ili iweze kuwa chanzo kikuu cha usambazaji wa umeme kwa Afrika Mashariki na ya Kati.

“Tunataka tuondokane na mgawo wa umeme na kuwa na umeme wa kutosha ambao hutasafirishwa nchi za jirani,” alisisitiza Katibu Mkuu huyo Jairo. Huku akiongeza kuwa hawatarajii kuwa na mgawo wa umeme wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Katibu Mkuu huyo alisema vyanzo vya umeme vitaendelezwa mfano vya maji ili kuifanya Tanzania iwe na umeme wa uhakika, tulivu na safi wenye bei nafuu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya hiyo Tarverdyan alisema mradi huo ni mkubwa katika uwekezaji wa nishati hiyo katika Afrika Mashariki, hivyo wamewekeza fedha hizo ili kubadilisha maisha ya Watanzania hususan walio kwenye eneo hilo .

Mahitaji halisi ya umeme nchini ni MW 897 wakati uzalishaji wa sasa ni zaidi ya MW 600.

No comments:

Post a Comment