USAJILI WA NAMBA ZA SIMU ZA MKONONI
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilitoa agizo kuwa namba zote za simu za mkononi zisajiliwe Kati ya Julai 1 2009 hadi Desemba 31, 2009; na baadaye muda huo kuongezwa hadi tarehe 30 Juni 2010 ikitamkwa wazi kuwa muda huo wa ujasili hautaongezwa tena.
Sababu za kuanzisha utaratibu wa
kusajili namba za simu zimeelezwa mara kadhaa zikiwemo :
Kuwalinda watumiaji dhidi ya matumizi mabaya ya huduma za mawasiliano
Kuwezesha na kurahisisha utambuzi wa wateja watumiapo huduma mbalimbali kama M – Pesa, Z-pesa, ZAP na huduma nyingine za malipo ya Ankara kama za Umeme, Maji, Televisheni n.k.
Kuimarisha usalama wa nchi.
Kuyawezesha makampuni ya simu kuwafahamu wateja wao vizuri zaidi ili kurahisisha na kuboresha utoaji wa huduma kwao.
Wakati tukikaribia tarehe 30 Juni utaratibu umepangwa kupitia makampuni ya simu kuwa kuanzia tarehe 1 Juni 2010 laini yoyote itakayonunuliwa itatumika kwa kupiga au kupokea simu na kutuma au kupokea ujumbe ikiwa imesajiliwa tu na si vinginevyo.
Baada ya saa sita usiku tarehe 30 Juni yaani saa 00.00 kuanzia tarehe 1 Julai, 2010 namba yoyote ambayo itakuwa haijasajiliwa itafungiwa kupiga ,kupokea simu pamoja na ujumbe wa maandishi (SMS) kwa siku 90 hadi tarehe 30 Septemba 2010. Katika kipindi hiki cha siku 90 endapo utaisajili namba yako itafunguliwa . Kwa namba ambazo hazitakuwa zimesajiliwa ifikapo tarehe 30 Septemba zitafutwa na kuondolewa kwenye mitandao kabisa.
Mnakumbushwa pia kuwa hivi karibuni mswada wa sheria ya mawasiliano ya kielektroniki na posta ulipitishwa na Bunge kuwa sheria. Sheria hiyo inafanya usajili wa namba za simu za mkononi kuwa ni wa lazima kwa mujibu wa sheria kuanzia sasa na kutofanya hivyo ni kosa la jinai.
Mamlaka ya Mawasiliano inapenda kuyashukuru makampuni ya simu na watumiaji kwa ushirikiano ambao mumeuonesha mpaka sasa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hili.
USICHELEWE, SAJILI NAMBA YAKO YA SIMU MAPEMA!
Imetolewa na
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
No comments:
Post a Comment