Wednesday, November 24, 2010

NCHI 56 DUNIANI ZATAJWA KUFANYA VEMA KATIKA KUUDHIBITI UKIMWI



NA MWANDISHI MAALUM

NEW YORK-Tanzania ni kati ya nchi 56 duniani ambazo zimefanikiwa ama kuudhibiti au kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa wa ukimwi kwa asilimia 25 katika kipindi cha kati ya 2001 hadi 2009.

Kati ya nchi hizo 56, 34 ni za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ripoti iliyotolewa jana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na mpango wa kupambana na Ukimwi ( UNAIDS) imeeleza kuwa kutokana na udhibiti wa ugonjwa huo, dunia hivi sasa imeanza kushuhudia kupungua kwa maambukizi mapya kwa asilimia 20 katika kipindi cha miaka 10.

Aidha taarifa hiyo pia inaeleza kuwa katika miaka mitano iliyopita idadi vya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo imeshuka kwa karibu asilimia 20 huku idadi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi ikitengamaa.

Kwa upande wa nchi tano ambazo kiwango cha maambukizo kilikuwa cha hali juu, nne kati ya hizo ambazo ni Ethiopia, Afrika ya Kusini, Zambia na Zimbabwe zimeweza kupunguza kwa asilimia 25 maambukizi mapya huku Nigeria ikielezwa kama iliyoweza kuimarisha kiwango cha maambukizi.

Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Afrika ndilo linaloelezwa katika ripoti hiyo kuwa ndio limeathirika zaidi kwa kuwa na asilimia 69 ya maambukizi yote mapya.

Hata hivyo ripoti hiyo imeonyesha kuwa nchi saba ambazo zote ziko katika Ulaya ya Mashariki na Asia ya Kati kiwango cha maambukizi mapya kimeongezeka kwa asilimia 25

Ripoti hiyo inabainisha zaidi kwamba vijana katika nchi 15 ambazo zimeathiriwa zaidi za ugonjwa huo, kiwango cha maambukizi mapya kimepungua kwa asilimia 25 hasa kutokana na vijana hao kutumia njia salama za kujamiana.

Takwimu zinaonyesha katika ripoti hiyo ambayo ni mpya, kuwa kwa mwaka 2009 idadi ya watu waliopata maambukizi mapya ilikuwa milioni 2.6 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 20 ilikilinganishwa na mwaka 1999 ambapo idadi ya watu walioambukizwa ilikuwa ni milioni 3.4.

Kwa mujibu wa ripiti hiyo watu waliokufa kutokana magonjwa yanayohusiana na ukimwi walikuwa 1.8 milioni kwa mwaka 2009 ikiwa ni pungufu ikilinganishwa na watu 2.1 milioni waliokufa mwaka 2004.

Ripoti hiyo inakwenda mbali zaidi kwa kuonyesha kuwa hadi mwishoni mwa mwaka 2009 watu 33.3 Milioni wanakadiriwa kuishi na virusi vya ukimwi, idadi ambayo ni juu kidogo ya watu 32.8 milioni kwa mwaka 2008.

Sababu ya kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wanaoishi na virusi inaelezea katika ripoti hiyo kuwa inatokana na watu hao kutumia dawa za kuudhibiti ugonjwa huo (ARVs)

Mkurugezi Mtendaji wa UNAIDS Bw. Michel Sidibe akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika Geneva Uswis anasema kuwa uwekezaji mkubwa wa raslimali na mipango madhubuti katika kupambana ugonjwa huo kumeza matunda.

Hata hivyo Bw. Sidibe anasema kumekuwa na upungufu katika ufadhili wa kimataifa katika mipango na miradi ya kupambana na ugonjwa huo, hali inayoweza kurudisha nyuma au hata kuzorotesha mafanikio hayo.

No comments:

Post a Comment