Friday, February 4, 2011

ISOME KATIBA YA TANZANIA.

Kutoka kushoto; Jaji Mkuu,Othman Chande, Spika wa Bunge,Anna Makinda,Rais wa Jamhuri ya Muungano,Jakaya Kikwete. Wana madaraka sawa?Katiba inasemaje?

Kama kungekuwepo na software ya kutambua neno au maneno ambayo kwa muda sasa yametawala vinywa na mijadala mbalimbali inayoendelea nchini Tanzania na hata nje ya nchi miongoni mwa watanzania, bila shaka maneno yafuatayo yangeshika nafasi za juu sana; Katiba ya Tanzania, Dowans,Tanesco,Mgao,Migomo, Bodi ya Mikopo,CHADEMA,CCM…
Kwa ujumla mijadala yote ni muhimu.Kadri tunavyojadiliana ndivyo tunavyopanua mawazo na kutafuta mbinu za kutatua masuala husika. Tatizo linakuja pale tunapojadiliana kwa jazba na kisha kuishia kulaumiana tu bila kuwa na mapendekezo halisi au huku wengine wakiona mijadala hiyo kama vitisho na hivyo kuamua kunyamazisha mijadala hiyo kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Miongoni mwa mijadala ambayo ni muhimu sana kuwa nayo au kuiendeleza ni pamoja na huu wa Katiba ya Tanzania.Kama tunavyoelewa,Katiba ya nchi ni mama na baba wa sheria zote.Katiba ndio nchi.Muongozo. Yapo maoni mbalimbali yanayoendelea; Je kuna haja ya kuibadili katiba iliyopo,kuiandika upya au kuiwekea tu viraka hii tuliyonayo ya mwaka 1977? Tuliyonayo inasema nini,ina kasoro gani?Mijadala kama hiyo.
Wasomi mbalimbali,wataalamu wa masuala ya katiba,wameshaanza kuchangia vizuri sana kuhusu mchakato huo.Mfano mzuri ni lile Kongamano la Katiba lililoandaliwa hivi karibuni pale University of Dar-es-salaam na kushirikisha wasomi,wakufunzi na wataalamu mbalimbali wa masuala ya katiba. Kama hukuwahi kuona japo video clips mbalimbali kutoka katika kongamano lile,nakushauri U-Google “Kongamano la Katiba” ujionee na kujifunza .
Lakini tunaposubiri kutangazwa rasmi kwa tume ya katiba(nilitumaini ingeshaanza kazi) kama alivyoahidi Rais Kikwete wakati wa salamu zake za mwaka mpya, ni wazi kwamba kazi kubwa ipo mikononi mwetu;wananchi. Kama Tume itakusanya maoni,itaweka vikao mbalimbali na wananchi na kujadili au kusikiliza mapendekezo kuhusu Katiba, kuna ulazima wa wananchi hao kujua kilichomo kwenye katiba ya sasa ambayo wengi tunataka ibadilishwe kwa sababu haiendani na wakati uliopo!
Hapo ndipo umuhimu wa kuisoma Katiba unapokuja.Kwa bahati mbaya,Katiba haifundishwi mashuleni. Wanaopata nafasi ya kujifunza katiba wakiwa darasani ni wale wanaosomea Constitutional Law katika ngazi ya vyuo. Huku chini ambapo ndipo walipo au walipoishia watanzania wengi, katiba haipo katika mitaala(curriculum).
Sitoshangaa wala kukulaumu msomaji wa post hii ukiniambia kwamba hujawahi kusoma hata kifungu kimoja kutoka ndani ya Katiba. Hukupewa nafasi.Maktaba ya shule uliyosomea haikuwahi kuwa hata na copy moja ya Katiba.Ufanyeje?
Bahati nzuri ni kwamba hivi sasa tunaishi katika zama za sayansi na tekinolojia. Leo hii katiba inaweza kusomeka kutoka katika simu ya kiganjani(mobile phone). Inasomeka katika computer na pia kuna machapisho mengi zaidi ya katiba. Ukienda kwenye duka la vitabu hivi leo,bila shaka utapata copy.
Tunachotakiwa ni kuisoma Katiba(kama hujawahi kuisoma),kuwasomea wenzetu ambao kwa sababu moja ama nyingine hawajapata muda au nafasi ya kuisoma.Na unapoisoma usiisome kama vile unavyosoma kitabu cha hadithi.Hiki ni kitabu cha marejeo(reference book).Unaweza kurejea katika vifungu fulani fulani kila mara kadri inavyohitajika.
Ushauri wangu ni kwamba ukishasoma ufafanuzi wa mwanzo kuhusu katiba,inavyoundwa nk, unaweza kurukia katika vifungu fulani fulani ambavyo unahisi vinakugusa zaidi. Kama wewe ni mtu unayependa kushiriki mijadala mbalimbali kwa kutoa maoni yako, tafuta kifungu kwa mfano kinachoongelea haki yako ya kutoa maoni. Kama suala la madaraka ya Rais(inasemekana katiba ya sasa inampa madaraka makubwa sana) dhidi ya madaraka ya Bunge na Mahakama soma vifungu vinavyohusiana na madaraka ya mihimili hiyo mitatu. Ukifanya hivyo,siku Tume ikifika kwako utakuwa na cha kuchangia. La sivyo…

No comments:

Post a Comment