Wednesday, March 9, 2011

Tamasha la Pasaka kurindima Dodoma, Shinyanga

Rose Mhando
Solomon Mukubwa
Upendo Nkone

Na Mwndishi wetu

TAMASHA kubwa la Pasaka baada ya kufanyia Dar es salaam April 24 mwaka huu, pia litafanyika katika mikoa ya Dodoma na Shinyanga.

Mwenyekiti wa kamati ya Msama Promotions waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama amesema kwamba mjini Dodoma litafanyika siku ya Aprili 25 ambayo ni Jumatatu ya Pasaka na Shinyanga litafanyika Aprili 26.

Jijini Dar es Salaam Tamasha hilo litafanyika sikukuu ya Pasaka Aprili 24 katika ukumbi wa Dimond Jubilee jijini Dar es salaam.

Awali tamasha hili lilipangwa pia kufanyika jijini Mwanza, lakini kutokana na sababu maalumu sasa litafanyika katika mikoa mitatu tu… yaani Dar es Salaam, Dodoma na Shinyanga.

“Tumebadilisha ratiba kidogo kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu hatutaweza kufanya tamasha hili jijini Mwanza,” alisema Msama.

Kwa mujibu wa Msama, Tamasha la Pasaka la mwaka huu lengo lake kubwa ni kwa ajili ya kukusanya fedha za kuwasaidia watoto yatima pamoja na mitaji ya wanawake wajane.

Aidha pia fedha zitakazofanyika katika tamasha hilo zitatumika kuwasaidia wahanga wa mabomu yaliyotokea katika kambi ya jeshi Gongo la Mboto jijini Dar es salaam.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha nchi sita ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, DR Congo, Afrika Kusini na Zambia.